Sisi ni nani?
Tarehe 01.01.1980 Askofu mstaafu Mathias Isuja Joseph aliahidi kujenga nyumba ya mapadre katika eneo la Parokia kusudi mapadre waweze kutoa huduma kwa waamini kwa urahisi. Nyumba hiyo ilianza kujengwa tarehe 7.05.1980 na ilibarikiwa tarehe 31.07.1980 ambayo ni sikukuu ya Mt.Inyasi wa Loyola. Idadi ya waamini waliozunguka eneo la kanisa iliongezeka na kufanya kanisa kuwa dogo, na hivyo kuamua kuanza kujenga kanisa jingine lililopo sasa. Ujenzi huo ulianza mwaka 1979 na kwa ushirikiano mzuri wa waamini na watu wenye mapenzi mema uliendelea vizuri. Ufadhili mkubwa wa kumaliza kanisa hili ulitolewa na Masista wa Mt. Petro Klaveri (Sisters of St. Peter Claver) waishio Roma, Italia. Hii ilipelekea kanisa hilo kuitwa la Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska ambaye ni mwanzilishi wa Shirika hilo la Masista. Ujenzi ulikamilika mwezi April, mwaka 1984. Utume wa walei kupitia Vyama vya kitume na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo unaimarishwa na muundo wa Halmashauri ya Walei ya Parokia inayowajibika na kuishi utume wake kulingana na katiba yake. Halmashauri inalo jengo lake ambalo lilizinduliwa na Mh. Askofu mstaafu Mathias Isuja Joseph Tarehe 27.10.2002. Hadi mwaka 2002 Parokia ilikuwa na Vigango vifuatavyo: Mpamaa, Chipondwa, Nzuguni Sokoine, Nzuguni Maweni, Ihumwa, Kizota, Makole, Nkuhungu na Miyuji. Parokia yetu imekuwa mzazi wa parokia zifuatazo:- Parokia ya Makole mwaka 2002, Parokia ya Nkuhungu mwaka 2005, Parokia Miyuji Mbwanga mwaka 2006 na parokia Ndogo ya Mt. Inyasi wa Loyolo (Miyuji Kusini) mwaka 2009. Parokia inavyo vyama vya kitume vifuatavyo na kila chama kadiri ya karama na utume wake husaidia katika shughuli za kitume. • Wafransiko Wasekulari • Wanawake Wakatoliki Tanzania ( WAWATA) • Wakarismatiki • Christian Professionals of Tanzania ( CPT) • Legio Maria • Moyo Mtakatifu wa Yesu • Vijana Wakatoliki ( Pia kuna vikundi vya Miito na Magis) • Shirika la Kipapa la Kimisionari la Utoto Mtakatifu • Wanaume Wakatoliki Kufikia mwaka 2009, Parokia ilikuwa na jumuiya 29 na Parokia Ndogo ya Mt. Inyasi wa Loyola ilikuwa na jumuiya 5. Hii ndiyo historia fupi ya Parokia ya K/Ndege Kanisa la Mwenye Heri Maria Teresa Ledochowaska. TUMSIFU YESU KRISTU.